Mengi ataja mafisadi papa 2009-04-24 14:38:18 Na Muhibu Said
Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, amewataja watu watano wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi mkubwa nchini na kuitaka serikali iwashughulikie haraka iwezekanavyo ili kuinusuru nchi kuyumbishwa nao. Watu hao, ambao Mengi alisema kwamba wanatuhumiwa kuwa ni `mafisadi papa`, ni pamoja na Mbunge wa Igunga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC-CCM) na Halmashauri Kuu ya Chama hicho (NEC-CCM) Taifa, Rostam Aziz. Aliwataja wengine, kuwa ni wafanyabiashara, Tanil Somaiya, Yusuf Manji, Jeetu Patel na Subash Patel, ambao alisema wanatuhumiwa kuiba mabilioni ya wananchi na kuzihamishia nje ya nchi. ``Hawa wanatuhumiwa kuiba mabilioni ya fedha za wananchi, na baya zaidi fedha hizo zimehamishiwa nje ya nchi,`` alisema Mengi alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za IPP Limited, jijini Dar es Salaam jana na kuongeza: ``…mafisadi wote na hasa wale wanaotuhumiwa kuwa mafisadi papa ni lazima washughulikiwe, la sivyo wataiyumbisha na kuitingisha nchi yetu. Ni lazima Watanzania tuone kwamba sasa tumefika mahali pa kusema imetosha.`` Alisema watu hao ni kati ya watuhumiwa wasiozidi kumi wanaotuhumiwa kwa ufisadi mkubwa nchini na kuongeza kuwa wanahusishwa na karibu kila kashfa kubwa nchini, ikiwamo inayohusu kampuni hewa ya Richmond, ambayo ilitiliana saini na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) mkataba tata wa kufua umeme wa dharura. Kashfa nyingine, ambayo watu hao wanahusishwa nayo, alisema inahusu Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambamo imethibitika kuchotwa Sh. bilioni 133 kwa njia za kifisadi na ile inayohusu kampuni ya Dowans Tanzania Limited, iliyorithi mkataba tata wa Richmond. Nyingine, inahusu ununuzi wa helikopta na magari ya jeshi, ndege ya Rais, rada, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSPF), Bahati Nasibu ya Taifa na Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma. Alisema jitihada kubwa za Rais Jakaya Kikwete za kuleta maendeleo na maisha bora kwa kila Mtanzania, zimekuwa zikidhoofishwa na wizi mkubwa wa rasilimali za taifa, huku Watanzania wengi wakiandamwa na umaskini mkubwa, ikiwamo kutojua hata mlo mmoja kwa siku utatoka wapi. ``Chakusikitisha ni kwamba, pale Mtanzania mwema mwenye uwezo anaposaidia jamii kuondokana na umaskini, mafisadi wanapiga kelele kuwa misaada ya aina hiyo ina agenda. Wanapinga, wanataka Watanzania wafe kwa njaa na matatizo mengine,`` alisema Mengi. Alisema inavyoonekana, nia ya watu hao ni kutaka kuvuruga nchi na kwamba, si ajabu wakaunga mkono matatizo yanayotokana na kampuni ya Development Enterpreneurship Community (Deci) iliyokuwa ikichezesha mchezo wa upatu na Watanzania wakabaki wakifukuzana na wachungaji bila kujiuliza ni kina nani hasa wanachochea vurugu hizo. Mengi alisema ‘mafisadi papa, hawawaibii tu Watanzania rasilimali, bali wanawaibia pia muda. ``Badala ya kutumia muda katika shughuli za maendeleo tunajikuta tukitumia muda mwingi kupambana nao, na hawatingishiki. Badala yake wanatumia fedha walizotuibia kuanzisha magazeti ya kujenga kiburi cha kutudharau, kututukana na kutunyanyasa. Inakuwa kesi ya mwizi kumkimbiza na kumpiga aliyeibiwa,`` alisema Mengi. Alisema hata hivi sasa, `mafisadi papa` wanaendelea kutumia uwezo wao wa kiuchumi uliotokana na wizi wa rasilimali za nchi kushawishi na kupata miradi mikubwa mikubwa kwa kutumia majina tofauti tofauti, huku wakipuuza kabisa kelele za wananchi kuhusu ufisadi huo. Mengi alisema Watanzania wanaolia na ufisadi, ni mamilioni wakiongozwa na Rais Kikwete, lakini wapo wachache waliojitokeza na wanajulikana kwa majina. Alisema zipo habari kwamba, wanaotuhumiwa kuwa `mafisadi papa`, wamedhamiria kuwatokomeza kabisa wanaopiga vita ufisadi wanaojulikana kwa majina. Kutokana na habari hizo, alisema: ``Mafisadi papa ni lazima wajue kwamba iwapo wapambanaji hao wa ufisadi watadhuriwa kwa njia yoyote hapa nchini au nje ya nchi, watawajibishwa na wananchi wa Tanzania.`` Aliongeza: ``Ni lazima Watanzania sasa tujiulize, hivi hawa mafisadi wanapata wapi ujasiri wa majigambo, dharau na nguvu za kututukana na kutunyanyasa?`` Awali, Mengi alisema nia njema ya Rais Kikwete ya kupambana na mafisadi na aina zote za uovu zimewashtua mafisadi na sasa wamecharuka na wanapambana na watu wote wanaomsaidia kupambana nao kuwazuia wasiendelee kuitafuna nchi. Rostam amekuwa akituhumiwa kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, inayodaiwa kuchota Sh. bilioni 40 kwenye EPA, tuhuma ambazo amekuwa akizikanusha. Shubash Patel anakabiliwa na sakata la kuchukua ardhi ya wanakijiji kwa njia za hila eneo ambalo kuna madini ya chuma, katika eneo la Mchuchuma, Iringa. Tanil Somaiya anatajwa kuwa ni mshirika kwa mtuhumiwa wa ununuzi wa rada, Shailesh Prapji Vithlani ambaye tayari ana kesi katika mahakama ya Kisutu alikoshitakiwa bila kuwepo nchini. Katika sakata la rada, serikali ililizwa kiasi kikubwa cha fedha huku zaidi ya Dola milioni 12 zikiingia katika mifuko ya waliofanikisha ununuzi huo. Somaiya na Vithlani walikuwa wanamiliki kampuni nchini iliyohusika na kashfa hiyo. Jeetu Patel kwa sasa ana kesi za EPA katika mahakama ya Kisutu zikihusu kampuni zake tano tofauti ambazo zilihusika kuchota mabilioni ya fedha kati ya Sh bilioni 133 zilizochotwa kifisadi.
SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako