Friday, April 24, 2009

Maximo Kuwatema Wazee

2009-04-24 14:02:56 By Jimmy Charles
Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo, amesema atawaacha wachezaji wakongwe kwenye kikosi chake atakachokitangaza leo. Kikosi cha Stars kinatarajia kutangazwa leo tayari kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Mabingwa wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani (CHAN), timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Stars, inatarajia kujipima ubavu na Kongo, Mei 9 kama maandalizi ya kujiandaa na mchezo mwingine wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya New Zealand utakaochezwa Juni 3, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam. Akizungunmza na Nipashe jana, Maximo alisema kuwa katika kuhakikisha anawaachia watanzania wachezaji watakaolitumikia taifa lao kwa muda mrefu, amedhamiria kuachana na wachezaji wenye umri mkubwa pamoja na wale wasiokuwa na nidhamu kuanzia kwenye klabu zao hadi kwenye timu ya taifa. Maximo, alisema kuwa kikosi chake kitakuwa na wachezaji wengi wenye umri mdogo, ambao atawachanganya na baadhi ya wachezaji wenye uzoefu lakini hawana umri mkubwa. Alisema kuwa kikosi chake kitawashtua watu lakini hilo halitampa tabu kwani malengo yake ni kutekeleza kile alichopanga kuifanyia Tanzania kabla ya kuachana nayo mwakani. ``Najua nitawashtua watu kwenye kikosi changu nitakachokitangaza Ijumaa, lakini sitajali, lengo langu ni kuhakikisha nawaachia watanzania hazina ya wachezaji,``alisema Maximo. Alisema vijana atakaowajumuisha kwenye kikosi chake watakuwa na kati ya umri wa miaka 18, 19, 20 hadi 28, ambapo kama mchezaji atakuwa amevuka kwenye umri huo atakuwa amepoteza sifa ya kuitwa kwenye kikosi chake. Baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha Maximo kilichokwenda Ivory Coast kwenye michuano ya CHAN ni Shaban Dihile, Deo Mushi, Shadreck Nsajigwa, Salum Swed, Amir Maftah, Juma Jabu, Godfrey Bony,Kigi Makassy,Athumani Idd, Henry Joseph, Mrisho Ngasa, Musa Mgosi,Mwinyi Kazimoto,Haruna Moshi na Jerry Tegete.
SOURCE: Nipashe

No comments:

Post a Comment