Naelewa ya kwamba nimeelemea upande mmoja kwenye swala zima la siasa ya Tanzania lakini si bila kuwa na sababu. Nitaorodhesha vichwa vya habari kutoka kwenye website ya CCM na mtu yeyote anayefikiri ninakosea kuviita vituko karibu unikosoe. Tuanzie na hiki kichwa cha habari "Tutawakopesha wavuvi zana za kuvulia " halafu nitanukuu maneno haya chini yake"RAIS Jakaya Mrisho Kikwete na Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu amesema kuwa endapo atachaguliwa tena ataanzisha mpango maalum wa kuwakopesha zana wavuvi katika maziwa ya Tanzania".

"Aidha, Rais Kikwete amewatangazia majambazi wanaofanya uharifu, kushambulia na hata kuua wavuvi katika maziwa ya Tanzania kuwa sasa kiama chao kimefika".Kweli? Umekaa madarakani miaka mitano leo hii ndio unawakumbuka hawa wavuvi? Utawarudisha wale waliouwa na majambazi? Hii ni aibu, Kusimama mbele ya watu na kuwadanganya kwamba utawasaidia wakikuchagua tena wakati muda wote huu hukuwajali.
Badala ya kuwachosha na maandishi yalioyobakia nitaviorozesha vichwa vya habari vilivyobaki ili niweze kurudi kwenye point muhimu.
"Mkutano wa Kampeni Makete: JK akaa vumbini na mlemavu wa viungo "
"Mkutano wa Kampeni Loliondo: JK aahidi kupunguza tatizo la maji Wilayani Ngorongoro"
"Mkutano wa Kampeni Ifunda – JK Awasihi Watanzania Kuepuka Siasa za Ubaguzi "

Watanzania wote wanashea UMASIKINI. Ndio kunawale wanasema hapana kunamatajiri bongo lakini waulize kama wanafurahia maisha yao? Huwezi kusema wewe ni tajiri na unamaisha mazuri lakini umeme unakatika kila leo sawa na msela wa uswazi,tofauti pekee unatumia jenereta. Huwezi kusema kunamatajiri wakati hawalali kwa amani kwa kuhofia majambazi. Huwezi kusema kuna matajiri wakati maji ya bomba hakuna wanategemea maji ya tank. Huwezi kusema kunamatajiri wakati wote tunabanana kwenye miundo mbinu mibovu.
Baada ya miaka yote hii ya kuwa chama tawala, miaka yote hii ya kutawala bunge. Ni kweli unaomba uchaguliwe tena uwape wakazi wa loliondo maji? wakazi wa Dar kwa ujumla na mikoa yote iliyobaki utawapa maji lini? Eti JK akaa mavumbini na mlemavu umuhimu wa hilo tukio ni nini? JK anasera gani za kuwalinda walemavu? hicho ndio kitu ningependa kujua na sio kukaa chini na mlemavu halafu unamuacha chini.
Bado sijapitia vyama vingine kuona sera zao ila I hope haziko rejareja namna hii. Watanzania inabidi tuache ushabiki wa kwenda kumshangilia mtu ambaye hana nia ya kuinyanyua nchi badala yake anakuja na wachekeshaji na wasanii wa kizazi kipya kukwepa maswala ya kweli yanayomkabili mwananchi. Ni muhimu kuamua kuchagua maendeleo badala nani alitudondoshea pati nzuri zaidi.