Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepata umaarufu mkubwa na kuandikwa zaidi na vyombo vya habari hapa nchini, baada ya kumteua Dk. Willibrod Slaa, kuwa mgombea wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huu.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kimepewa nafasi kubwa ya kuandikwa katika kipindi hiki cha kampeni zilizoanza Agosti 20 mwaka huu kuliko vyama vingine hapa nchini.
Hayo yamebainika katika utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Kimataifa ya Synovate na matokeo yake kutolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, kabla ya kutangazwa mgombea huyo, Chadema kilikuwa kikiandikwa katika magazeti, kutangazwa kwenye redio na kuonyeshwa katika runinga mbalimbali hapa nchini kwa kiwango kidogo .
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusiana na utafiti huo, Meneja wa Huduma za Wateja wa Synovate, Jane Meela, alisema katika utafiti wao wamebaini kuwa baadhi ya vyombo vimeandika habari zao kwa haki, vingine kwa kupendelea chama kimoja na vilivyobaki havikuwa upande wowote. Alisema vyombo vingi vya habari vya serikali, chama na vile vya binafsi vilikiandika zaidi CCM kuliko vyama vingine vya siasa .
Aliongeza kuwa taasisi yake ilifanya utafiti kwa kuangalia vituo 10 vya runinga, magazeti 36 na vituo vya redio 31 katika mikoa tofauti nchini.
Aidha, utafiti huo umebaini kuwa suala la amani lilijadiliwa na watu mbalimbali kwa asilimia 28, rushwa 21, uchumi 15, elimu 12, kilimo saba, afya sita, watu wasiojiweza sita, haki za binadamu tatu na utalii na ajira vilishika nafasi sawa kwa kupata asilimia moja.
Taasisi hiyo pia hufanya utafiti wa masuala mbalimbali yanayohusu jamii na kutoa matokeo yake kwa vyombo vya habari.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment