Kwa kawaida hakuna kipindi cha muhimu kwa nchi yoyote ya mfumo wa kidemokrasia kama kipindi cha uchaguzi mkuu. Kwa nchi nyingi zenye kufuata mfumo huu, kipindi cha uchaguzi kina maana ya wakati wa kuchagua mwelekeo mzima wa nchi kwa kipindi kinachofuata cha uongozi.
Kwa nchi nyingi za kiafrika huu sio ukweli sahihi. Kipindi cha uchaguzi mkuu kimekuwa ndio kipindi cha wasiwasi kwa wananchi wengi. Ni kawaida kabisa kwenye bara hili kwa kampeni kuambatana na vitisho, wanasiasa kukamatwa na polisi, vurugu na umwagaji wa damu na baada ya uchaguzi si jambo la kushangaza kwa jeshi kuchukua nchi.
Kwa nchi nyingi za kiafrica ambazo zilikuwa kwenye siasa ya chama kimoja ni chache sana ambazo zimefanikiwa kubadili chama tawala. Ingawa mara nyingi lawama zinazotolewa ni za wizi wa kura lakini mara nyingi ni ukweli wa kwamba vyama pinzani haviwezi kushindana na chama tawala. Mfano wa nchi kama Tanzania, kuna vyama karibu ishirini, na chama kimoja kati ya vyote kinaweza kusema kimejikita katika kila kijitongoji cha nchi nzima na nacho ni CCM. Kwa miaka takribani thelathini CCM ndio kilikuwa chama pekee. Ndani ya kipindi hiki chama na serikali kilikuwa ni kitu kimoja. Wananchi wote waliokuwa na imani na serikali walikuwa na imani na chama. Asilimia kubwa ya hao wananchi wanaendelea kuwa imani na chama chao leo hii. Na bila kizazi hicho cha wanachi kuweza kubadilika itachuwa muda mpaka uchaguzi mkuu wa Tanzania kuwa na maana. Tanzania itabidi isubiri mpaka kizazi kipya kizidi namba ya kizazi cha zamani.
Pamoja na kwamba tasmini yangu inaonyesha kwamba swala mabadiliko ya chama tawala ni swala lisilowezekana Tanzania kwa muda huu lakini sio kweli kwamba haliwezekani kabisa. Uwezekano upo kama vyama vya upinzani vingeweza kuungana na kutoa upinzani wa kweli. Ninaposema kuungana simaanishi kusimamisha mgombea mmoja kwa vyama vyote bali ni kuunganiasha vyama vyote na kubaki na chama kimoja chenye nguvu. Kama hilo litawezekana basi mabadiliko yatawezekana.
No comments:
Post a Comment