Serikali imesema kuwa kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kuboresha hospitali za mikoa kufikia kiwango cha rufaa ili ziweze kutoa huduma zitokanazo na ajali kubwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, alitoa kauli hiyo wakati akizindua ripoti ya kuzuia ajali kwa watoto.
Nyoni alisema kuwa serikali imeamua kuboresha hospitali hizo kutokana na kwamba wagonjwa wengi wanaopata ajali kubwa husafirishwa kutoka mikoa yao kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) katika Taasisi ya Mifupa (MOI).
Alisema hospitali za mikoa zikiboreshwa vizuri, zitakuwa zinatoa huduma bora kama zitolewazo na MNH na hatua hiyo itasaidia kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika hospitali hizo.
Hata hivyo alisema kuwa suala hilo litasaidia kwa wagonjwa kupatiwa huduma bora kwa haraka zaidi kuliko kusubiri kusafirishwa katika mkoa mwingine kwa ajili ya matibabu.
Alisema bado kuna uhaba wa madaktari bingwa wa upasuaji wa vichwa ambapo kwa sasa serikali inawaanda wataalamu wengine kwa ajili ya kuziba pengo hilo.
“Kama mnavyoelewa suala la madaktari bingwa wa upasuaji wa vichwa wapo wachache kwa hapa nchini, nadhani hawazidi watano hivyo bado kunahitajika wataalamu wengine ambao kwa sasa wanaandaliwa,” alisema Nyoni.
Alisema kumekuwepo na ajali nyingi zitokanazo na vyombo vya barabarani ambazo zimekuwa zikitokea kwa uzembe wa madereva ambao hawafuati sheria.
Nyoni alisema kuwa zaidi ya watu 2800 hufariki dunia katika ajali za barabarani kila mwaka ambapo kwa siku ni watu sita hadi nane na anapokufa mtu mmoja zaidi ya watu10 hupata majeraha na wengine ulemavu.
Nyoni alisema serikali imeliangalia
suala hilo kwa upande wa watoto kutokana na kwamba idadi kubwa ya ajali zimekuwa zikiwaathiri watoto.
“Ajali nyingi zimekuwa ni za watoto na hivyo serikali imebidi kuangalia suala hilo kwa upande wa watoto kutokana na kwamba ni taifa la kesho hivyo tumeamua kufanya tahadhari mapema,” alisema.
Alisema changamoto inayoikabili serikali kwa sasa ni kutoa elimu kwa wananchi ili wajihadhari na ajal hizo.
Alisema madereva wa pikipiki wanaathirika zaidi kutokana na kuendesha bila kuvaa kofia.
Hata hivyo, alisema elimu hiyo pia itatolewa kwa wanafunzi ili wawe na uelewa wa jinsi ya kujikinga na ajali wakiwa wadogo.
Mkurugenzi Mtendaji wa (MOI), Profesa Laurence Museru, alisema kwa sasa ajali zimeongezeka na kwamba nyingi zinatokana na usafiri wa pikipiki.
Kutoka Nipashe
No comments:
Post a Comment