Saturday, July 17, 2010

Meya muuaji bado kesi haijaiva.

Kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Leonald Bandiho Bihondo, pamoja na watuhumiwa wenzake watatu imepigwa kalenda kwa mara ya tano jana, huku ikielezwa kuwa sampuli ya damu ya aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Isamilo, marehemu Bahati Stephano (46), imepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.

Mwanasheria wa Serikali mkoani hapa, Patrick Donasian, alitoa maelezo hayo mahakamani jana wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Katika kesi hiyo ambayo watu wengi walihudhuria wakiwemo ndugu wa watuhumiwa, watumishi wa Halmashauri na ya Jiji la Mwanza pamoja na baadhi ya wafanyabiashara maarufu jijini hapa, Donasian alidai kwamba upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

“Mheshimiwa hakimu, ninaomba mahakama yako tukufu itaje tena kesi hii kwa sababu upelelezi wake bado haujakamilika,” alisema Donasian.

Alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoani hapa, Eugenia Rujwahuka, kwamba ofisi yake inaendelea na taratibu za upelelezi wa kesi hiyo, ikiwa ni pamoja na kupeleka sampuli ya damu ya marehemu Bahati Stephano kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Hakimu Rujwahuka alikubaliana na ombi la wakili wa serikali na kuamua kuwa kesi hiyo namba 16/2010 ije tena mahakamani hapo Julai 30, mwaka huu kwa kutajwa.
Kutoka Nipashe.


Katika kesi hiyo, Bihondo anatetewa na wakili wa kujitegemea, Deo Mgengele.

Marehemu Bahati Stephano aliuawa Mei 14, mwaka huu saa 6:30 mchana kwa kuchomwa na kisu akiwa ofisini kwake na kufariki wakati akikimbizwa kwenda Hospitali ya Rufaa Bugando kwa matibabu.

Washitakiwa wengine ni Jumanne Oscar, mkazi wa mkoa wa Kigoma ambaye anadaiwa kumchoma kisu marehemu, Baltazar Shausi pamoja na Abdu Ausi ambao ni wakazi wa kata ya Isamilo jijini Mwanza.

Wote wanashtakiwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya marehemu Bahati Stephano.

Bihondo ambaye amemaliza muda wake wa udiwani wiki iliyopita, baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani Jiji la Mwanza, alikamatwa Mei 19 mwaka huu, wakati akiwa kwenye uwanja wa ndege Jijini Mwanza, baada ya kutajwa na watuhumiwa wenzake.

No comments:

Post a Comment